Katika sehemu ya kwanza ya makala Kifo Cha Mende, tuliangazia baadhi ya visa vya mauaji ya kiholela na watu kutoweka kwa njia tatanishi nchini Kenya katika miaka ya hivi karibuni. Licha ya matukio haya kuongezeka na ushahidi kuashiria yanatekelezwa na vyombo vya usalama, idara ya usalama ingali inashikilia kuwa haihusiki kwa vyovyote vile.

Kauli hii ya idara ya usalama ni wimbo unaoudhi na kuchukiza masikioni mwa familia za wahasiriwa na yeyote mwenye nia safi na moyo mweupe. Ikiwa maafisa wa usalama hawahusiki, kwa nini hawafanyi uchunguzi na kukomesha matukio haya ilhali imo ndani ya uwezo wao kufanya hivyo?

Mustakabali wa Kenya

Mustakabali wa taifa la Kenya uko hatarini iwapo vyombo vya dola vitaendelea kuvunja sheria na kukiuka haki za binadamu bila hatua yoyote kuchukuliwa. Matokeo yake yasiyoepukika ni ujenzi wa utamaduni wa watu kufanya watakavyo, hata ikibidi kuua, almuradi wapate watakacho. Iwapo Kenya itafikia kiwango hiki, basi itakuwa imepoteza utaifa wake na kusalia kuwa sehemu tu ya ardhi isiyofunikwa na maji. Historia itakapoandikwa, tendo la serikali iliyopo sasa la kufadhili mauaji ya kiholela na kupotea kwa watu litaandikika kwa wino usioweza kufutika.

Japo serikali ya Kenya haitangazi hadharani kuwa inashiriki katika kuwaua na kuwapoteza watu, sio siri kwamba inafanya hivyo kwa kisingizio cha kuukabili uhalifu. Haiwezi kuwa sadfa kwamba wahasiriwa karibu wote walikuwa washukiwa wa uhalifu au ugaidi. Lisiloeleweka ni kwa nini serikali inakaidi sheria na kutumia njia ya mkato kuwaajibisha washukiwa. Kwa nini wasipewe haki ya kujitetea mahakamani kama inavyoamuru katiba? Kisheria, mshukiwa hana makosa mpaka mahakama itakapompata na hatia.

Serikali inayohukumu washukiwa

Utawala wa Rais Uhuru Kenyatta umejitwika jukumu lisilo lake la kuwahukumu washukiwa na kuitekeleza hukumu hiyo pasipo kuchelea. Inasikitisha kwamba hili linafanyika chini ya uongozi wa Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto ambao waliwahi kuwa washukiwa wa uhalifu dhidi ya binadamu.

Mojawapo ya mashtaka yaliyowakabili kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai mjini The Hague, Uholanzi ni mauaji ambayo yalitokea wakati wa ghasia zilizofuatia uchaguzi mkuu wa mwaka 2007. Baada yao kufika mahakamani na kukanusha mashtaka, ilibainika hatimaye kwamba hapakuwa na ushahidi wa kutosha. Kilichofuatia ni kufutwa kwa mashtaka hayo na kesi zao kutamatishwa.

Maswali yasiyo na wa kuyajibu

Je, ingekuwaje kama Kenyatta na Ruto wangehukumiwa moja kwa moja kuwa wana makosa bila hata kupewa nafasi ya kujitetea? Kwa nini washukiwa wa ugaidi au uhalifu wowote ule wasifikishwe mahakamani na sheria iachiwe ichukue mkondo wake?

Haya ni baadhi tu ya maswali ambayo yametawala fikira na mawazo ya familia za wahasiriwa kwa muda mrefu. Maswali ambayo hawapati wa kuyajibu. Waendapo kulala hawapati usingizi. Watapataje usingizi wakati maisha yao yamejaa uchungu na huzuni?

Isichofahamu serikali ya Rais Kenyatta ni kuwa kukithiri kwa visa vya mauaji ya kiholela na watu kutoweka kumeibua hasira na kinyongo mioyoni mwa familia, jamaa, na marafiki wa wahasiriwa. Hili limewapa msukumo wa kutaka kulipiza kisasi na kuwafanya washawishike upesi kujiunga na makundi ya ugaidi kama vile Al-Shabaab. Hatimaye wametumika kutekeleza mashambulizi ya kigaidi katika nchi yao. Ni kweli kunao waliopotoshwa na mafunzo yenye itikadi kali, lakini mzalendo mwenye akili timamu atalishambuliaje taifa lake?

Taswira katika Kifo cha Mende

Mfano hai wa taswira hii unadhihirika wazi katika makala ya upekuzi Kifo cha Mende. Katika miaka ya hivi karibuni, makumi ya watu wakiwemo wahubiri wa kiislamu wameuawa au kutoweka katika pwani ya Kenya. Baadhi yao ni Sheikh Aboud Rogo aliyeuawa Agosti 27, 2012, Sheikh Ibrahim Rogo aliyeuawa Oktoba 3, 2013, na Sheikh Abubakar Shariff maarufu “Makaburi” aliyekufa mnamo Aprili 1, 2014. Itakumbukwa kuwa Makaburi alikuwa ametoa usemi kwamba atauawa hapo kabla.

Mwengine aliyepoteza uhai wake mwaka wa 2014 ni Hassan Nasrulla Musa maarufu kama “Guti”. Guti aliuawa mnamo Novemba 8 katika barabara ya Mwembe Tayari akisafiri kwenye gari pamoja na mkewe. Wote hawa walimiminiwa risasi na watu ambao vyombo vya habari vilisema “hawajulikani”. Inaaminika mauaji yao yalitekelezwa na maafisa wa idara ya usalama kikiwemo kikosi cha kupambana na ugaidi.
Kutokana na mauaji haya na mengineyo, vijana wengi kutoka eneo la pwani wameenda nchini Somalia na kujiunga na wanamgambo wa Al-Shabaab. Hili limewaacha wazazi wao na hasa wa kike katika upweke na dhiki isiyodirikika.

Daima wanaishi kwa wasiwasi. Hawajui ikiwa watoto wao wako hai au wamekufa. Cha kusikitisha, hawawezi kwenda kwa vyombo vya usalama na kuripoti kwamba wanao wamepotea. Hii ni kutokana na kuhusika kwa maafisa wa usalama katika visa hivi. Maisha ya wazazi hawa yamekuwa taabu. Kwao, mbele hakwendeki na nyuma hakurudiki.

Mmoja wa wazazi waliothiriwa ni Fatma Mohammed. Mwanawe wa kiume kwa jina Mohammed Ali na ambaye alikuwa tegemeo lake la kipekee maishani aliondoka bila kumuaga. Tangu wakati huo, Fatma amekuwa akifanya kazi ya kuwapikia watu vyakula katika mtaa wa Majengo, Mombasa ili akimu mahitaji yake. Fatma hayuko pekee. Anawakilisha mamia ya watu katika jamii zilizoathiriwa kwa njia moja au nyingine na mauaji ya kiholela na kutoweka kwa watu.

Mwengine aliyeathirika japo sio kwa njia ya moja kwa moja ni John Kariuki, mchimba mawe kutoka Kaunti ya Nyeri. Yeye ni manusura wa shambulizi la kigaidi lilotekelezwa na kundi la Al-Shabaab mjini Mandera mnamo Disemba 2014. Watu 36 walifariki katika shambulizi hilo. John alipigwa risasi mgongoni na kwenye mikono. Ingawa ana uwezo wa kutembea, hawezi kufanya lolote kwa mikono yake kwani imelemaa. Chakula hukilia sahanini kwani hana uwezo wa kushika kijiko. Maji huyanywa akitumia mrija. Kwake kila kunapokucha ni heri ya jana.

Masaibu ya John, Fatma na maelfu ya Wakenya wengine yangezuilika ikiwa serikali ya Kenya ingekoma kujipiga kifua na kuukabili ugaidi na uhalifu kwa njia ipasayo. Ni lini serikali itabaini kuwa atupaye tope humrukia mwenyewe?

 

Na Dennis Mbae

Let the world know:

Africa Uncensored

View all posts

Add comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *